BREAKING NEWZ FROM TANZANIA GOVERNMENT, READ HERE>>>

By  

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Kama inavyofahamika, tangu mwezi Aprili mwaka jana, nchi yetu imekuwa ikipokea raia toka Burundi wanaoingia nchini kuomba hifadhi ya ukimbizi kutokana na hali ya machafuko iliyotokea nchini mwao.

Hadi kufikia tarehe 10 Februari, 2016, kiasi cha wakimbizi 129,210 toka nchini Burundi wamepokelewa nchini.

Kati ya hawa, wakimbizi 79,290 wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu mkoani Kigoma. Wengine 45,487 wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyoko wilayani Kibondo na 4,543 wanahifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya Mtendeli iliyoko wilayani Kakonko mkoani Kigoma.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na wadau wengine imekuwa ikitoa huduma muhimu kama vile za afya, chakula, maji na ulinzi ili kuhakikisha kuwa wakimbizi hawa wanaishi kwa usalama.

Hata hivyo, ukiacha wakimbizi hawa walioanza kuingia nchini mwezi Aprili 2015, Tanzania bado ina wakimbizi wengine ambao wapo katika Kambi ya Nyarugusu. Katika kambi hiyo kuna Wakongo 61,887, Wasomali 150 na wengine 189 toka nchi mbalimbali. Hii ina maana kuwa hadi kufikia tarehe 10 Februari, 2016 nchi yetu ilikuwa na jumla ya wakimbizi 191,436 ambao wamehifadhiwa katika makambi.

RAIA WA NJE WALIOOMBA HIFADHI NCHINI

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pia imeendelea kushughulikia raia wa nchi za nje ambao baada ya kuingia hapa nchini wameomba kupatiwa hifadhi ya ukimbizi.

Hadi sasa maombi 815 ya waomba hifadhi yameshashughulikiwa na Kamati ya Kitaifa ya Kuwahoji Waomba Hifadhi (NEC).

Kati ya hawa, 735 wametoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, 25 wametoka nchini Burundi, 14 wametoka nchini Rwanda na 15 wametoka nchini Yemen. Wengine 18 wametoka nchini Syria, 3 Iran, 2 Kenya na 3 wametoka nchini Eritrea.

Hawa wote maombi yao yameshashughulikiwa na matokeo yatatolewa hivi karibuni baada ya uchambuzi yakinifu kukamilika.

Maombi mengine 147 pia yamepokelewa na hivi karibuni Kikao cha NEC kitakaa kujadili maombi yao.

Kati ya hawa raia 24 wametoka nchini Yemen, 13 Syria, 3 Somalia, 6 Rwanda na 18 kutoka DRC. Wengine 2 kutoka Uganda, 1 kutoka Sudan Kusini na 80 kutoka nchini Burundi.

Kundi hili la waomba hifadhi ni wakimbizi ambao waliingia nchini kabla ya mwezi Aprili, 2015.

Pamoja na kuwafahamisha wananchi na wadau wengine kuhusu hali ya wakimbizi nchini, Taarifa hii pia inatolewa ili kuweka sawa habari potofu zilizoandikwa katika ukurasa wa kwanza wa gazeti la This Day toleo la tarehe 15 Februari, 2016 kuwa Tanzania ina wakimbizi 1,960,000 na kuwa 63,000 kati ya hawa, wengi wao kutoka Syria na Yemen, wameomba hifadhi Tanzania. Taarifa za gazeti hili sio za kweli.

IMETOLEWA NA ISAAC J NANTANGA

MSEMAJI - WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI.