CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimetia mpira kwapani kwa kukimbilia mahakamani baada ya kuona mazingira ya kushinda Ilala na Kinondoni hayawezekani kwa namna yeyote. Zoezi la uchaguzi ambalo lilipaswa kwenda sambamba na uapishwaji wa Madiwani wa Manispaa ya Kinondoni na Ilala umeahirishwa kwa zuio la Mahakama ya Kisutu.
Akisoma zuio hilo Mwanasheria wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Burton Mahenge amesema amepokea zuio hilo leo asubuhi lililojumuisha Manispaa zote mbili za Kinondoni na Ilala. Ingawa baada ya kuongea na waandishi wa habari hawakueleza imekuwaje Mahakama ikatoa zuio siku ya Jumamosi, tena mahakama ya Kisutu kupinga amri iliyotolewa na mahakama kuu ijumaa kwa kesi hiyo hiyo kuhusu uchaguzi wa manispaa hizo.
Mahenge amesema zuio hilo lenye jarada la MISC Civil Application Na 7 ya mwaka 2016 na kupewa kesi ya madai ya msingi Na. 1 ya mwaka 2016 haikueleza sababu za zuio hilo kwa kuwa imesikilizwa upande mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi huo amesema, kesi hiyo ya madai imefunguliwa na Elias Phiremon Nawera mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiitaka mahakama kusitisha uchaguzi wa Ilala na Kinondoni.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Aron Kagurumjuli mara baada ya kuahirishwa kwa mkutano huo amesema,
“Agizo la mahakama niliipokea jana saa 12 jioni, hivyo nikashindwa kuwajulisha wajumbe kuwa hakutakuwa na mkutano kutokana na muda. Sina budi kutii amri ya mahakama kwani ningeendeleza mjadala ningekiuka sheria”.
Alipoulizwa ilikuwaje akapokea zuio hilo usiku saa 12:00 na wakati haukuwa muda wa kazi, alisema yeye huwa anafanya kazi usiku na mchana, ana muda wa kuingia ofisini hana muda wa kutoka.
Aidha amesema, zuio hilo la mahakama lilitolewa jana na kupelekwa ofisi kwake jioni. Hivyo kesi hiyo itasikilizwa January 13 mwaka huu mahakamani hapo.
“Mimi siwezi kuhoji sana kwanini Mahakama kuu iliruhusu shughuli hii ifanyike leo halafu mahakama ndogo ya Kisutu leo imetoa zuio, mimi natii agizo la mahakama hadi pale itakapo sikiliza kesi hiyo na kutoa uamuzi”, amesema Kagurumjuli.
Uchunguzi uliofanywa na mwanahalisi online, umebaini kuwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) nao tayari walishaleta wabunge wa viti maalumu kutoka Zanzibar na Pemba ili kuikabili vema CCM iliyoleta wabunge kutoka Zanzibar kwa ajili ya kupiga kura Kinondoni. Hadi jana asubuhi Ukawa walikuwa na madiwani 44 dhidi ya CCM iliyokuwa na 31 katika uchaguzi huo.
CCM iliingia pamoja na Mawaziri wawili, Makame Mbarawa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Pamoja na Augustine Mahiga Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kikanda na kimataifa ambao kwenye kikao cha awali kilichoahirishwa hawakuwepo.
Wakati huo huo, Mbunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Saed Kubenea Amesema kuwa, wamesikitishwa sana na kilichotokea leo kwani hawakutarajia.
Kubenea amesema, wanatarajia kwenda mahakamani siku hiyo ya kusomwa kesi na kusikia sababu za kesi hiyo kufunguliwa. “ Tunauhakika mtu aliyefungua kesi hiyo hana mamlaka iwaje mwananchama wa kawaida afungue kesi tena asiyekuwa mkazi wa kinondoni?”.
“Baraza la Madiwani kinondoni halipo tangu mwezi wa saba mwaka jana je wananchi wataishi vipi bila uongozi wa chini? tunawasiwasi na mahakama zetu kujihusisha na mambo ya kisiasa. Sisi hatutakubali tutafuatilia hadi tupate haki yetu kwani ushindi ni wetu,” amesema Kubenea.
CREDIT: MWANAHALISI ONLINE
CREDIT: MWANAHALISI ONLINE